Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Dkt. Mahdi bin Ahmad al-Sumaydai, Mufti wa Jamhuri ya Iraq, katika ujumbe wake kwa Waziri Mkuu wa Iraq kuhusu kusitishwa safari za ndege kati ya Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesisitiza umuhimu wa kulinda mamlaka ya Iraq, kuhakikisha maslahi ya wananchi wa nchi hiyo na kuzuia tofauti za kisiasa zisigeuke kuwa shinikizo dhidi ya mataifa, ujumbe huu pia umetumwa mahsusi kwa Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun.
Al-Sumaydai, huku akisisitiza heshima kamili kwa mamlaka ya Serikali ya Iraq na haki ya serikali kuchukua hatua kwa ajili ya kulinda usalama na maslahi ya nchi, alisema kwamba; mamlaka ya Iraq haipaswi kumaanisha kuigeuza nchi hii kuwa uwanja wa kutekeleza matakwa ya wengine, na wala wananchi wa Iraq hawapaswi kubeba gharama za migogoro na sera ambazo hazitumiki kwa manufaa yao.
Akizungumzia ukweli kwamba Iraq ni nchi ya Kiislamu na uwepo wa uhusiano wa kidini, ujirani, historia na maslahi ya pamoja kati ya mataifa ya Kiislamu, kuhusu uhusiano wa Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: “Iran ni nchi jirani ambayo ina mpaka wa pamoja na Iraq, pamoja na uhusiano wa kina wa kijamii, kiuchumi na kidini.”
Mufti wa Jamhuri ya Iraq aliendelea kwa kuuliza: “Inawezekanaje kuzuia taifa la Kiislamu kusimama pamoja na Iraq katika mazingira magumu, halafu Iraq ikaombwa ilichukulie taifa hilo kama upande unaopigana nayo?” Akasisitiza kwamba; tofauti za kisiasa hazipaswi kusababisha uadui kati ya mataifa.
Vilevile, alikumbusha misimamo ya nchi na mataifa yaliyosimama pamoja na Iraq katika vipindi vigumu ilivyopitia, hususan katika kukabiliana na kundi la Daesh (ISIS), na kutoa aina mbalimbali za msaada. Alisema kwamba matokeo ya misaada hiyo hayapaswi kuwa kufungwa milango dhidi ya raia wa nchi hizo na kuwabebesha madhara ya maamuzi ya kisiasa raia wasiokuwa wanajeshi, wagonjwa, wanafunzi na mazuwari.
Al-Sumaydai alifafanua kwamba; kauli yake haimaanishi kutoa wito wa kuvunja sheria, kupinga maamuzi ya kimataifa au kupuuza mamlaka ya Iraq, bali anataka sera ya Kiiraq inayolinda heshima ya Iraq na maslahi ya wananchi wake, na wakati huohuo kuzuia madhara kuwafikia wale waliosimama pamoja na nchi hii katika nyakati za migogoro iliyopitia Iraq.
Akisisitiza kwamba uaminifu ni miongoni mwa sifa za watu wenye heshima, na kwamba haki haiwezi kugawanywa, aliongeza kwamba; tofauti za kisiasa hazipaswi kugeuka kuwa uadui dhidi ya mataifa, na kwamba raia wasiokuwa wanajeshi hawapaswi kuadhibiwa kwa sababu ya sera za serikali zao.
Mufti wa Jamhuri ya Iraq aliendelea kwa kuitaka Serikali ya nchi hiyo kuweka maslahi ya Iraq mbele na kutumia njia zote za kidiplomasia na kisheria zilizopo ili kuzuia madhara ya migogoro ya kimataifa visiiathiri Iraq na wananchi wake.
Vilevile, alitaka juhudi zifanyike ili kutenga mazingira ya kibinadamu, kidini, matibabu na kielimu, na akasisitiza kwamba; viwanja vya ndege vya Iraq havipaswi kugeuzwa kuwa chombo cha kuawekea mataifa shinikizo.
Al-Sumaydai katika sehemu nyingine ya ujumbe wake alisemaa: “Mtu ambaye alisimama pamoja na Iraq katika nyakati za migogoro iliyopitia nchi hii, angalau anastahili kutendewa uadilifu, uaminifu na mwenendo unaostahili; na yeyote aliyeidhuru Iraq na wananchi wake, anapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria na haki, bila hatua za kisiasa kugeuka kuwa adhabu ya pamoja dhidi ya mataifa ya Kiislamu yenye uhusiano wa kidini na wa ujirani na Iraq.”
Aliendelea kusisitiza kauli hii kwa kusema: “Iraq kwanza, mamlaka ya Iraq kwanza, maslahi ya wananchi wa Iraq kwanza, na haki kwa wote—hiyo ndiyo njia yetu.”
Alisema kwamba haipaswi kuruhusiwa nyakati zijazo kujaa mshangao ambao hautakuwa na manufaa kwa wale ambao hawasikii sauti ya wananchi wa Iraq wala kuhisi maumivu na mateso yao.
Mufti wa Jamhuri ya Iraq pia, akizungumzia moyo na hisia za wananchi wa Iraq, alisema: “Wairaqi, kama walivyo na uzalendo na utayari wa kuilinda nchi yao, pia wana uaminifu na uzalendo kwa wale waliosimama pamoja nao na kuwasaidia katika nyakati za matatizo.”
Sheikh Mahdi al-Sumaydai mwishoni, kwa kurejea aya za Qur’ani Tukufu, alimuomba Mwenyezi Mungu ailinde Iraq na wananchi wake, aihifadhi nchi hii dhidi ya fitina na migogoro, na awaongoze na kuwarekebisha viongozi kwa ajili ya yale ambayo ndani yake kuna kheri ya nchi na wananchi.
Maoni yako